Maafisa wa Halmashauri ya kukabiliana na Pombe na Mihadarati (NACADA), wamewakamata washukiwa watano wakiwa na lita 55,000 za pombe haramu aina ya Kang’ara na lita 500 za chang’aa, kaunti ya Kisii.
Kulingana na halmashauri hiyo, watano hao wanaojumuisha wanaume watatu na wanawake wawili, walikamatwa katika operesheni kali iliyotekelezwa Alhamisi asubuhi katika kijiji cha Mwaguto, kaunti ndogo ya Kisii Kusini, kaunti ya Kisii.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa, alisema operesheni hiyo ni ufanisi mkubwa katika vita dhidi ya pombe haramu, akionya kuwa wale ambao watapatikana wakiendesha biashara hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
“Huu ni ujumbe kwa wale wanaotekeleza biashara hii kwamba, chuma chao ki motoni,’ alionya Omerikwa.
Aidha, Omerikwa alisema kuwa NACADA imeanzisha mchakato wa kisheria utakaosababisha ardhi hiyo ya ekari nne ambapo pombe hiyo ilipatikana, kutwaliwa na serikali.
“Eneo hili ni eneo la uhalifu na tutahakikisha inatwaliwa na serikali, kama njia moja ya kuangamiza biashara hiyo kabisa,” aliongeza Dkt. Omerikwa.
Washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani, huku NACADA ikiimarisha operesheni dhidi ya pombe haramu kote nchini.