Washukiwa watano wakamatwa kwa wizi wa shilingi Milioni 450

Tom Mathinji
1 Min Read

Tume ya kukabiliana na ufisadi hapa nchini EACC, imewakamata washukiwa watano kati ya 13, wanaohusishwa na wizi wa shilingi Milioni 450 katika idara ya urekebishaji tabia.

Washukiwa hao wanadaiwa kutekeleza ubadhirifu huo kati ya mwaka wa kifedha wa 2016/2017 na 2017/2018, kupitia usambazaji hewa wa bidhaa.

Kupitia kwa taarifa leo Alhamisi, tume ya EACC ilisema washukiwa hao walitumia kampuni 17 zilizohusishwa nao, kusambaza chakula kwa magereza mbali mbali, huduma ambazo hazikutolewa.

Miongoni mwa washukiwa hao ni pamoja na Sarah Kemunto Kerandi ambaye ni afisa mkuu wa fedha, Moses Juma Sirengo, mhasibu Mkuu, Jack Nyariango Ogao, Mhasibu, Maureen Ndungwa aliyetajwa kama mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hizo na Eric Kipkurui Mutai ambaye ni mfanyikazi katika kitengo cha usafi katika idara ya urekebishaji tabia, aliyetajwa kuwa mkurugenzi katika mojawepo ya kampuni hizo iliyopokea shilingi Milioni 267 ya fedha hizo.

Tume hiyo iliwataka washukiwa wanane ambao inawasaka, wajisalimishe katika makao makuu ya EACC Jijini Nairobi kufikia Ijumaa Julai, 19, 2024 saa mbili asubuhi.

Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha katika makao makuu ya EACC, wakisubiri kufikishwa mahakamani Ijumaa Julai 19, 2024.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article