Maafisa wa polisi, wamewakamata washukiwa wanne wanaoaminika kushiriki biashara haramu ya mihadarati, kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Kwenye msako wa pamoja uliotekelezwa na asasi mbali mbali za usalama kati ya tarehe 5 na 7 mwezi Octoba mwaka huu, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, iliripoti kuwa kitengo cha kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, kilimkamata kiongozi wa genge hilo Rishad Abdulrahim Sheikh, na binamuye Hajinur Yussuf Mohamed walikamatwa katika kituo cha kibiashara cha Nyali, mjini Mombasa. Wawili hao wanahusishwa na Jesse Da Mata Dos Santos, ambaye ni raia wa Uingereza, aliyekamatwa Jijini Londona akiwa gramu 20 za Cocaine.
Washukiwa wengine wawili walikamatwa Jijini Nairobi ambao ni Muamar Mutua Mohammed na Adam Omari wanaodaiwa kuwa washirika wa Rishad Abdulrahim.
Wakati wa kukamatwa kwa washukiwa hao Mombasa na Nairobi, maafisa wa usalama walipata gramu 750 za Cocaine ya thamani ya shilling milioni 2.9 pamoja za vifaa vinavyotumiwa kuficha mihadarati.
Kwenye taarifa, kitengo cha kukabiiana na uhalifu wa kimataifa kilisema kilifanikiwa kuvunja sakata hiyo ya ulanguzi wa mihadarati inayoendeshwa kupitia uwanja wa ndege wa JKIA iliyowezesha kukamatwa kwa washukiwa hao wanne.
Washukiwa hao wametajwa katika ulanguzi wa cocaine inayoingizwa katika masoko ya humu nchini na ya kimataifa.
Washukiwa hao wamefikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya JKIA Njeri Thuku.
Maafisa wa uchunguzi walipewa idhini ya kuwazuilia hadi tarehe 29 mwezi huu, wakati kesi hiyo itakaposikizwa.