Washukiwa wa wizi wa magari wakamatwa Naivasha

Boniface Musotsi
2 Min Read

Maafisa wa usalama mjini Naivasha wamewatia nguvuni washukiwa watano wa wizi baada ya kupatikana na magari matatu yaliyoibwa na vifaa vya kielektroniki.

Kwa mujibu wa naibu wa kamishina wa kaunti ya Nakuru Mutua Kisilu, maafiisa kutoka vikosi mbalimbali vya usalama walinasa magari hayo aina ya Toyota fielder, Nissan Dualis na lori katika kaunti za Narok na Nakuru.

Aliongeza kuwa zipo taarifa kwamba washukiwa hao waliwaibia watu wakiwa kwenye sare za polisi na hata kuwajeruhi.

Katika kisa kimoja, jamaa akiwa kwenye mavazi ya polisi, alimteka nyara mwanamke mmoja katika eneo la Mirera mjini Naivasha na kutumia gari lake kusafirisha vifaa vya kielektroniki vilivyoibwa.

Vile vile, imeripotiwa kuwa jamaa fulani aliomba kubebwa na dereva wa gari la mizigo ila baadaye akamgeuka njiani, akamjeruhi na kumwibia mwenye gari maelfu ya pesa.

Kisilu aliwapongeza polisi kwa juhudi zao za kupambana na visa hivyo hasa wizi wa nyumbani ambao katika siku za hivi karibuni, wezi wamekuwa wakivunja milango,kuwawateka watu nyara na kuitisha fidia, kuwajeruhi na kuwaibia vifa vya kielektroniki.

Pia alisema kuwa vikosi vya usalama vinafuatilia kwa karibu hali za usalama kwenye barabara ambapo magari ya mizigo ya masafa marefu yamekuwa yakitekwa nyara na wizi kutekelezwa.

Alishukuru umma kwa kupiga ripoti na kutoa maelezo muhimu kuhusu visa hivyo ambayo yamesababisha kupatikana kwa mali iliyoibwa na kunaswa kwa baadhi ya wahusika ambao wameshtakiwa.

Kwa upande wake, OCPD Stephen Kirui alisema kuwa tayari washukiwa watano wa genge la wezi wamekamatwa na kushtakiwa.

Boniface Musotsi
+ posts
Share This Article