Washukiwa 7 wa mauaji ya mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Afrika Kusini Kiernan Jarryd Forbes maarufu kama AKA na rafiki yake Tebello Motshoane maarufu kama Tibz wamekamatwa.
Taarifa kutoka kwa maafisa wa polisi nchini Afrika Kusini inaashiria kwamba washukiwa watafikishwa mahakamani kesho Alhamisi.
Wanajumuisha wawili waliofyatua risasi, watatu waliotumwa kufuatilia AKA, mmoja ambaye alitafuta silaha zilizotumika ambazo ni bunduki na wa mwisho ndiye alipanga mchakato mzima.
Awali polisi walitangaza kukamatwa kwa washukiwa sita Jumanne jioni huku wa saba akikamatwa leo Jumatano asubuhi. Wengine kati yao wanahusishwa na visa tofauti vya mauaji.
AKA na rafiki yake Tibz waliuawa kwa kupigwa risasi nje ya mkahawa mmoja jijini Durban Februari 10, 2023. Inaaminika kwamba siku hiyo mwimbaji AKA alifuatwa na washukiwa kutoka uwanja wa ndege wa Durban hadi eneo la tukio.
Mpaka sasa kilichochochea mauaji hayo hakijabainika lakini polisi wanasema wanafahamu kwamba Tibz hakuwa mlengwa katika kisa hicho.