Mahakama imewapata washukiwa sita na kosa la mauaji ya aliyekuwa mbunge wa Kabete George Muchai, walinzi wake wawili na dereva.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani Lucas Onyina alisema sita hao Erick Munyera, Raphael Kimani, Mustafa Kimani, Stephen Asitiva, Jane Wanjiru na Margaret Njeri, pia wanakabiliwa na mashtaka mengine ya wizi wa mabavu pamoja na kumiliki bunduki na risasi bila kibali.
Upande wa mashtaka ulibaini kuwa usiku wa Februari 6 na 7, 2025, washukiwa hao waliwaibia Michael Ngatia, Gladys Waithera na Irene Muthoni katika matukio tofauti, huku wakitishia kutumia nguvu dhidi yao.
Wakati wa kutekeleza wizi huo, washukiwa hao waliiba mali ya tamani ya shilingi Milioni 1.1, ambayo ilijumuisha magari mawili, mtungi wa gesi, simu nne za mkononi, tarakilishi na pesa taslimu.
Washukiwa hao walipatikana na makosa baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi 36, ambao ushahidi wao uliwahusisha washukiwa na uhalifu huo.
Mahakama itatoa vifungo vyao Machi,18 2026.