Serikali inatoa wito kwa raia kutoa taarifa zikazosaidia kuwakamata washukiwa 35 wa ugaidi wanaotuhumiwa kwa kutekeleza mashambulizi katika kaunti ya Lamu na eneo la Boni kwa jumla.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki anasema washukiwa hao wanasakwa kuhusiana na kuhusika kwao katika uwekaji wa vilipuzi kwenye barabara kadhaa za eneo hilo, mauaji ya raia kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen na pia katika maeneo ya Lango la Simba, Witu, Mpeketoni, Juhudi, Salama na Hindi miongoni mwa mengine.
Kindiki pia anawatuhumu kwa kutekeleza shambulizi kwenye kambi ya kijesji ya Marekani katika eneo la Manda Bay Januari 5, 2020.
“Washukiwa, ambao majina na picha zao zitachapishwa katika magazeti makuu nchini na kupachikwa katika mitandao rasmi ya kijamii ya Wizara ya Usalama wa Kitaifa na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Oktoba 18, 2023, wanaagizwa kujisalimisha kwa kituo chochote cha polisi ndani ya Jamhuri ya Kenya mara moja,” anasema Waziri Kindiki katika taarifa.
Anaongeza kuwa kitita kikubwa cha fedha kitatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazosaidia kuwakamata washukiwa hao 35.
Serikali imetangaza vita vikali dhidi ya magaidi yaliyojihami kwa silaha yaliyo na uhusiano na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab.