Wasanii Tanzania watoa jumbe za pole kwa waathiriwa wa ghasia

Marion Bosire
2 Min Read
Ben Pol

Wasanii mbali mbali nchini Tanzania wametoa jumbe za pole kwa raia wenzao wa taifa hilo ambao walipoteza wenzao wakati wa ghasia zilizozuka kufuatia uchaguzi mkuu.

Mwanamuziki Benard Michael Paul Mnyang’anga maarufu kama Ben Pol ameandika, “Kama Mtanzania, moyo wangu una hisia nzito. Kwa siku chache zilizopita, tumepoteza ndugu, dada, kina mama, kina baba na marafiki.”

Aliendelea kusema kwamba taifa la tanzania linahuzunika pakubwa kutokana na hilo huku akitakia kila familia ambayo inaomboleza faraja.

Kulingana na Pol, waliofariki sio hesabu tu bali walijaa kusudi, ndoto na simulizi akiongeza, “Mwenyezi Mungu na afariji kila boma inayoomboleza na nyoyo za walioaga zilazwe pema penye amani ya milele.”

Nandy naye alichapisha ujumbe mfupi kwenye Insta Story ambapo alisema, “Natoa pole za dhati kwa familia, ndugu na Watanzania wote. Mungu awape faraja waliopoteza wapendwa wao, na atupe sote hekima, amani na umoja kwa taifa letu katika wakati huu”.

Ripoti za mitandaoni zilionyesha awali kwamba Nandy na familia yake waliathirika na maandamano ya baada ya uchaguzi ambapo waandamanaji wanaripotiwa kupora duka la mume wake Billnass ambaye pia ni msanii wa muziki.

Huku hayo yakijiri, msanii mkongwe wa Bongo Fleva nchini Tanzania Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, ameshangzwa na wasanii wanaoendelea kuchapisha challenge za nyimbo zao mitandaoni wakati huu Watanzania wenzao wamepoteza ndugu jamaa na marafiki akishangaa wanajisikiaje??

Website |  + posts
Share This Article