Emmanuel Wanyonyi ndiye Mkenya pekee aliyeibuka mshindi wa tuzo ya Almasi katika siku ya pili na ya mwisho ya mkondo wa 14 wa Diamond League maarufu kama Prefontaine Classic Jumapili usiku mjini Eugene nchini Marekani.
Wanyonyi alimshinda bingwa wa dunia Marco Arop wa Canada kwa mara ya pili mtawalia katika 800 akikata utepe kwa dakika 1 sekunde 42 nukta 80.
Arop alimaliza wa pili dakika 1 sekunde 42 nukta 85.
Bingwa wa dunia Mary Moraa aliambulia nafasi ya 4 katika mita 800 nyuma ya Athing Mu wa Marekani, Keely Hodgkinson wa Uingereza na Natoya Goule wa Jamaica waliofuatana katika nafasi za 1, 2 na 3 mtawalia.
Beatrice Chebet alimaliza wa pili katika mita 5,000, akiweka muda wa tatu wa kasi duniani wa dakika 14 sekunde 5 nukta 92.
Gudaf Tsegay wa Ethiopia aliibuka mshindi huku akivunja rekodi ya dunia yake Faith Kipyegon ya dakika 14 sekunde 5 nukta 20, akinakili dakika 14 na nukta 21.
Katika matokeo mengine ya jana Jumapili usiku, Andre de Grasse wa Canada na Shericka Jackson wa Jamaica waliibuka washindi katika mita 200.
Mondo Duplantis wa Uswidi aliweka rekodi mpya ya dunia katika urukaji kwa upote akiruka umbali mita 6 nukta 2.
Kwa jumla, Wakenya watatu wishinda mataji ya almasi wakiwa Faith Kipyegon katika mita 1,500, Simon Koech katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji na Emmanuel Wanyonyi katika mita 800.