Wanne wakamatwa na EACC kwa tuhuma za kutumia vyeti bandia

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imewakamata watu wanne kwa kuchuma mali kwa kutumia vyeti bandia vya masomo. 

Wanne hao ni Edna Bitange ambaye ni Afisa Msaidizi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Mark Sandui Chebiwey ambaye ni mfanyakazi wa Tume ya Ugavi wa Mapato, CRA, Francis Njiru Mfundi ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Biashara Ndogo na Brenda Nelly Sulungai ambaye ni Msaidizi wa Maendeleo ya Jamii katika kampuni ya Maji na Maji Taka ya Nairobi City.

Msemaji wa EACC Eric Ngumbi anasema wanne hao walikamatwa jana Jumatano na kufikishwa katika kituo cha polisi cha tume hiyo ili kuandikisha taarifa.

Watafunguliwa mashtaka mbalimbali ya kughushi vyeti vya masomo.

EACC imeimarisha msako dhidi ya watu waliotumia vyeti bandia kupata ajira serikali, msako ambao hadi kufikia sasa umesababisha kukamatwa kwa watu kadhaa.

Kulingana na tume hiyo, kuna watumishi wa umma zaidi ya 2,000 walioajiriwa kwa kutumia vyeti bandia.

Share This Article