Ziara ya Rais William Ruto katika eneo la Nyanza, haitasababisha wakazi wa eneo hilo kusitisha ufuasi wao kwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, hayo ni kwa mujibu wa kiongozi wa wachache katika bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi.
Mbunge huyo alisema kuwa eneo hilo linamuunga mkono kikamilifu kiongozi huyo wa Azimio la Umoja, akiongeza kuwa makaribisho aliyopewa Rais Ruto katika eneo hilo ni jambo la kawaida.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Ugunja Jumamosi, Wandayi alitoa wito kwa wanasiasa wa chama cha UDA katika eneo hilo kuheshimu uongozi wa Nyanza na pamoja na wakazi wake.
“Eneo hilo linamuunga mkono kikamilifu kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement ODM, Raila Odinga” alisema Wandayi.
Aidha Wandayii alisema miradi inayozinduliwa katika eneo hilo ni duni kwa wakazi wa eneo hilo.
“Rais Ruto anapaswa kuacha baadhi ya miradi hiyo kuzinduliwa na Magavana na wawakilishi wadi,” alisema Wandayi.
Matamshi ya Wandayi yanajiri huku Rais William Ruto akifanya ziara ya kimaendeleo ya siku nne katika eneo la Nyanza.
Rais atazuru kaunti za Kisumu, Homa Bay, Migori na Siaya, ambako atazindua miradi ya maendeleo.