Wanawake wapongezwa kwa mchango wao katika kujenga nchi

Rais Ruto alisema hayo katika mkutano na wanachama wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Ikulu ya Nairobi.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumatano amesifia wanawake kwa mchango wao mkubwa katika ujenzi wa taifa.

Ruto amesema hayo alipohutubia mkutano wa wanachama wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Ikulu ya Nairobi.

Kulingana naye, wanawake hujibidiisha sana kazini akitoa mfano wa wanawake wanaohudumu kama mawaziri ambao alisema wanatekeleza kazi zao vyema hata kushinda wenzao wa kiume.

Rais alitoa wito wa kulainishwa kwa mipango ya chama hicho ili kuhimiza umoja nchini.

Aliahidi mchango wa shilingi milioni 90 pesa ambazo zitatumiwa kulipa ushuru ambao chama cha Maendeleo ya Wanawake kinadaiwa na milioni 250 zitakazosaidia kuanzisha chama cha ushirika cha akiba na mikopo.

Ahadi nyingine aliyotoa kiongozi wa nchi kwa chama hicho ni kuweka mradi wa nyumba za gharama nafuu kwenye ardhi yao.

Katika mkutano huo, wanachama wa chama hicho walimwomba Rais Ruto kuhakikisha kwamba sheria ya usawa wa kijinsia ya theluthi mbili inatekelezwa kikamilifu bungeni.

Mlezi wa chama hicho Beth Mugo, alisema kwamba inahuzunisha kuona kwamba bunge limeshindwa mara kadhaa kupitisha sheria zitakazosaidia katika utekelezaji wa sheria hiyo, hata baada ya mwingilio wa mahakama.

Waziri wa Ardhi Alice Wahome, ambaye ni mwanachama wa kudumu wa chama cha Maendeleo ya Wanawake, alisema iwapo itatekelezwa, sheria ya uwakilishi sawa wa kijinsia ya theluthi mbili itaimarisha ushirikishaji na utawala.

Rais Ruto alihakikishia wanawake hao kwamba atawasiliana na bunge ili kutafuta suluhisho la utekelezaji wa sheria hiyo.

Share This Article