Kundi moja la wanawake kutoka kaunti ya Meru, limeunga mkono kuidhinishwa kwa waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya.
Wanawake hao waliokusanyika katika uwanja wa Kinoru mjini Meru, walielezea imani yao na utendakazi wa waziri Kindiki.
Walitoa wito kwa wenzao wa Mlima Kenya Magharibi, kuungana nao kumuidhinisha waziri kindiki.
Wakati huo huo, wanawake hao walisema wanamuunga mkono Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, wakitaja hatua ya hivi majuzi ya kumbandua mamlakani kuwa yenye nia mbaya.
Matamshi hayo ya wanawake hao yanajiri siku chache baada ya baraza la wazee wa Njuri Ncheke kutangaza kuwa Kindiki ndiye msemaji mpya wa Mlima Kenya, katika sherehe iliyoandaliwa katika madhabahu ya Ncheru, Tigania Magharibi kaunti ya Meru.
Aidha wazee hao pia walitoa wito wa umoja kati ya Mlima Kenya Magharibi na ile ya Mashariki, ili kufanikisha maendeleo.