Wanaume 3 walazwa hospitalini baada ya kupigwa na radi Narok

Martin Mwanje
1 Min Read

Wanamume watatu wamelazwa hospitalini baada ya kupigwa na radi wakati wakilisha ng’ombe katika kijiji cha Kileleshwa, kaunti ndogo ya Narok Kusini.

Wawili kati ya watatu hao walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Narok huku mmoja akitibiwa kwenye hospitali ya Longisa, kaunti ya Bomet.

Naibu kamishna wa kaunti ya Narok Felix Kisalu alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa watatu hao walikuwa wakilisha ng’ombe katika shamba la Jonathan Letina.

“Walikuwa wamekimbizwa kwanza katika hospitali ya kaunti ndogo ya Ololulunga ambako walihamishwa hadi hospitali ya rufaa. Walikuwa wakilalamikia maumiivu ya kifua na mgongo,” alisema.

Alitoa wito kwa wakazi wachukue tahadhari kwa kuepukana na maeneo yanayokumbwa na radi hususan wakati huu wa mvua.

Aidha, alizirai shule za sehemu hiyo kuweka vifaa vya kuzuia radi katika majengo yao kwa kuwa eneo hilo hukumbwa na radi.

Mwaka uliopita, watu watatu walipoteza maisha katika eneo hilo kwenye visa tofauti vya kupigwa radi.

Share This Article