Chama cha wanasheria nchini LSK kimemwandikia waraka kamanda wa polisi katika eneo la Nairobi Adamson Bungei, kikimtaka aruhusu maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 kuendelea.
“Tumeona taarifa yako kwa umma leo ambapo unasema kwamba umetupilia mbali maandamano yaliyopangwa na hivyo kuhujumu haki ya wananchi kuandamana kwa njia ya amani na bila silaha.” ulisema waraka huo wa LSK ukiendelea kwamba hatua hiyo ya Bungei ni kinyume cha sheria.
Wanasheria hao wamefafanua kwamba katiba katika kifungu nambari 37 inakubalia wananchi kukusanyika na kuandamana na haisemi lolote kuhusu kumjuza au kumpa notisi kamanda wa polisi kabla ya maandamano.
Waliendelea kunukuu kifungu nambari 19 cha katiba sehemu ya tatu ambayo imeorodhesha haki na uhuru wa wananchi na hatua alizochukua Bungei ni sawa na kutupilia mbali sehemu hizo za katiba jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
LSK imemtaka Bungei kubatilisha usemi wake na badala ya kuingilia waandamanaji ahakikishe polisi wametoa ulinzi kwa waandamanaji jijini Nairobi wanaolalamikia mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Iwapo atakosa kuridhia matakwa yao, wanasheria hao wametishia kumshtaki kamanda huyo wa polisi Nairobi mahakamani na kuhakikisha anawajibikia mabaya yote ambayo yatawafanyikia waandamanaji.
Taarifa hiyo ya LSK imetiwa saini na rais wa chama hicho Faith Odhiambo, naibu rais Mwaura Kabata pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.
Ilitolewa baada ya ripoti kuashiria kwamba waandamanaji walikuwa wanakamatwa na maafisa wa polisi jijini Nairobi.