Wanaofuzu kutoka TVET kuajiriwa katika miradi ya serikali

Tom Mathinji
2 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, amesema kuwa wanafunzi wanaofuzu kutoka kwa vyuo vya mafunzo ya kiufundi, TVET, watakuwa katika mstari wa mbele kutekeleza na kufanikisha miradi ya serikali.

Akizungumza katika kaunti ya Nyeri leo Ijumaa, naibu huyo wa Rais  alisema taasisi za TVET zinatekeleza wajibu muhimu kuwapa vijana ujuzi wa kufanikisha miradi kama ule mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

“Ujuzi mnaopata kutoka kwa taasisi za TVET, utatumika vyema katika mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Tunawahitaji masoroveya, wahandisi, mafundi wa stima na maseremala miongoni mwa wengine, ili kufanikisha mradi huo,” alisema naibu huyo wa Rais.

Aliongeza kuwa taasisi za TVET zimetekeleza wajibu muhimu katika kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapa ujuzi wa kiufundi, utakaowawezesha kupata mapato.

“Utawala wa Rais Ruto unatambua uwezo wa TVET  wa kuwawezesha vijana hadi katika maeneo ya mashinani. Hii ndio sababu tunapanua taasisi hizo kuhakikisha kuna TVET moja katika wakilishi wadi zote 1,450 kote nchini,” alisema Gachagua.

Na ili kuhakikisha wakenya zaidi wanapata ujuzi wa kiufundi, Gachagua alisema serikali itajenga taasisi mpya 16 za TVET katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

“Hatua hii kutokana na kuajiriwa kwa zaidi ya wakufunzi 2,000, huku tukilenga kuwaajiri wakufunzi 4,000,” aliongeza naibu huyo wa Rais.

Website |  + posts
Share This Article