Wananchi walalamikia ukataji ovyo wa miti katika misitu ya Nyandarua

Lydia Mwangi
2 Min Read

Wakazi wa Kaunti ya Nyandarua wamezua malalamiko makubwa dhidi ya shughuli zinazoendelea za ukataji miti katika misitu ya eneo hilo, wakisema kuwa shughuli hizo zimeharibu miundombinu ya barabara na kuhatarisha mazingira.

Barabara zilizowekwa lami na zile ambazo hazijawekwa zimeathirika vibaya.

Barabara za lami zimeanza kupata mashimo marefu kutokana na magari mazito yanayosafirisha magogo, huku barabara zisizokuwa za lami zikigeuka kuwa mashimo na kupitika kwa shida kubwa.

Dkt. Lucas Gacheru, mkazi wa Nyandarua Kusini ambaye pia ni mwakilishi wa wakulima na jamii ya wafanyabiashara wa Kinangop, ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua kali dhidi ya ukataji huo.

Aidha, amehimiza bunge kuanzisha sheria itakayohakikisha kwamba wananchi wa Kinangop wananufaika kwa angalau asilimia 40 ya mapato yanayotokana na uvunaji miti unaofanywa katika eneo lao.

Dkt. Gacheru pia alielezea hali ya kusikitisha ya wakazi wa Njabini, ambao licha ya kuwa walinzi wa Bwawa la Sasumwa—chanzo muhimu cha maji kwa jiji la Nairobi—hawapati faida yoyote kutokana na uwepo wake.

Katika upande wa Nyandarua Magharibi, Tom Ndiritu ambaye ni mwana mazingira kutoka Ol Joro Orok alielezea masikitiko yake kuhusu ukataji miti kabla ya miti hiyo kukomaa.

Alitoa mfano wa msitu wa Gathanji ambao, kulingana naye, umekatwa wote kwa mfululizo, hali iliyowaacha wakazi wakiwa na mshangao.

“Tunaendelea kupanda miti kama sehemu ya juhudi za kitaifa za upandaji miti, ilhali wengine wanakata miti hiyo kiholela,” alisema Ndiritu.

Alipoulizwa kuhusu hali ya ukataji miti katika misitu ya Nyandarua, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Misitu nchini Kenya (KFS), Alex Lemarkoko, alieleza kuwa jukumu la KFS ni kupanda miti na kuitunza hadi ikomae.

Alikanusha madai kuwa KFS hushughulika na utoaji wa zabuni kwa wakata miti au wamiliki wa mashine za kukata mbao.

Vilevile, alikanusha madai kwamba miti inayokatwa kwa sasa inahusiana na miradi ya serikali ya nyumba za bei nafuu, akisema kuwa “hayo ni madai yasiyo na msingi wowote.”

Hata hivyo, wakazi bado hawajaridhishwa na majibu hayo, na wanaendelea kutaka uwazi na uwajibikaji zaidi katika usimamizi wa misitu ya kaunti hiyo.

Lydia Mwangi
+ posts
Share This Article