Wananchi waandamana kulalamikia ukosefu wa maendeleo Tanzania

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi wa maeneo yaliyo karibu na hifadhi ya wanyamapori ya Ngorongoro nchini Tanzania ambao wengi ni wa jamii ya Maasai waliandamana na kufunga barabara ya kuingia kwenye hifadhi hiyo.

Waliozungumza na wanahabari walisema kwamba maandamano yao ya amani ni ya kushinikiza serikali itatue matatizo yanayowakabili.

Wananchi hao wa Tanzania walisema waliamua wenyewe kuchukua mkondo wa maandamano ya amani na hawana kiongozi kwani hawaamini viongozi.

Wanalalamikia masuala kama kutokarabatiwa na kutojengwa kwa shule ambapo nyingi hazina vyoo faafu hali ambayo inaweka wanafunzi na walimu katika hatari ya kupata magonjwa kama kipindupindu.

Kiwango cha juu cha ushuru ni suala jingine lililosukuma watu hao kuandamana na wanataka jibu kwa malalamiko yao litoke kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe.

Wanasema Rais ndiye alitamka kwa mara ya kwanza suala la Ngorongoro na ndiye Amiri Jeshi Mkuu na ndiyo sababu wanataka awajibu.

Kulingana nao, hii sio mara ya kwanza wakazi wa Ngorongoro wanapeleka malalamishi kwa Viongozi wa ngazi ya juu kabisa wa kitaifa, wakirejelea wakati walimlalamikia makamu wa rais Philip Mpango huko Loliondo.

Wanasema mbunge wao aligusia matatizo yao katika mkutano huo na hakujibiwa.

Wameapa kusalia kwenye barabara kuu ya kuingia kwenye hifadhi ya Ngorongoro hadi pale ambapo watapata jibu mwafaka kutoka kwa serikali.

Share This Article