Wananchi nchini Tanzania wameanza rasmi zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Maeneo mengi nchini humo yalianza shughuli hiyo kwa utulivu, huku wananchi katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Zanzibar, na Tanga wakiripotiwa kufika kwenye vituo vya upigaji kura mapema.
Maafisa wa uchaguzi katika maeneo hayo wanasema vituo vimefunguliwa kwa wakati, na kuhimiza kufuatwa kwa taratibu zote ikiwemo uhakiki wa wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR).
Baadhi ya wapiga kura wameeleza kufurahishwa na maandalizi ya tume na kuhimiza wananchi wenzao kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba.
Awali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (INEC) ilitoa wito kwa wapiga kura kutokaa majumbani na kuendelea kujitokeza hadi muda wa kufunga vituo utakapofika saa 10:00 jioni.
 
					 
				 
			 
                 
                                
                              
		 
		 
		 
		