Maafisa wa polisi katika kaunti ya Mandera wanawasaka washukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, ambao waliharibu mtambo wa mawasiliano wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, katika eneo la Sukela Tinfa katika kaunti hiyo.
Wananchi wametakiwa kuwa macho na kuripoti watu wanaowashuku kwa maafisa wa usalama.
Wavamizi hao ambao walitekeleza uharibifu huo mwendo wa saa saba unusu jana Jumatano usiku, walitumia vilipuzi kuharibu mtambo huo, hali iliyosababisha kutatizika kwa mawasiliano ya simu katika eneo hilo.
Maafisa wa usalama wamesema hatua zimechukuliwa ili kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.
Mnamo wiki iliyopita, gari la uchukuzi wa umma lililokuwa likisafiri kutoka Elwak lilishambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab kwenye barabara ya Elwak-Rhamu-Mandera, ambapo abiria kadhaa walijeruhiwa.