Wanajeshi wa UN kuondoka DRC kufikia mwisho wa mwaka huu

Marion Bosire
2 Min Read

Wanajeshi waliotumwa katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC na Umoja wa Mataifa, UN kusaidia kudumisha amani nchini humo wataondoka kabisa kufikia mwisho wa mwaka huu.

Walitumwa huko kupambana na makundi yaliyojihami ya wapiganaji zaidi ya miongo miwili iliyopita na sasa wakati umewadia kwao kuondoka.

Kamanda wa kikosi hicho cha MONUSCO Bintou Keita alizungumza kwenye mkutano na wanahabari jijini Kinshasa ambapo alithibitisha hilo.

Tangazo la kamanda Keita linajiri baada ya serikali ya taifa hilo kutaka kikosi hicho kiondoke kwa sababu ya kile ilichokitaja kuwa kushindwa kulinda raia dhidi ya waasi.

Makundi ya waasi kama vile M23 yamekuwa yakihangaisha raia wa DRC hasa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo kwenye mikoa kama Kivi Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

Wanajeshi hao wataondoka katika awamu tatu ambapo 2,000 wataondoka Kivu Kusini kufikia mwisho wa Aprili na vituo vyao kuchukuliwa na wanajeshi wa DRC.

Watafuatiwa na walio kwenye mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri kufikia mwisho wa mwezi Disemba kulingana na Waziri wa Mambo ya nNe wa DRC Christophe Lutundula.

Lutundula alifafanua kwamba kuondolewa kwa kikosi cha MONUSCO hakumaanishi kwamba vita dhidi ya waasi vitafikia mwisho bali ni njia ya kutetea uhuru na himaya ya taifa hilo.

Serikali ya DRC iliagiza pia kuondoka kwa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichokuwa kimetumwa nchini humo kusaidia kupambana na waasi.

Kikosi hicho cha EACRF kilikuwa kimehudumu nchini DRC kwa muda wa mwaka mmoja tu.

Share This Article