Wanajeshi wa EACRF waanza kuondoka DRC

Marion Bosire
1 Min Read

Wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, EACRF wameanza kuondoka mashariki ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC baada ya serikali ya nchi hiyo kuonyesha kutoridhika na ufaafu wa jeshi hilo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ilituma kikosi hicho DRC kufuatia ombi la serikali ya nchi hiyo Novemba 2022 baada ya kurejea kwa kundi la waasi la M23, lengo likiwa kuondoa waasi hao katika sehemu walizokuwa wameteka.

Baadaye, Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliomba kikosi hicho kiondolewe kwa madai ya kushirikiana na waasi badala ya kuwaodoa.

Katika mkutano wa viongozi wa EAC Novemba 25, 2023, ilitangazwa kwamba DRC iliamua kutoongeza muda wa kikosi cha EACRF baada ya Disemba 8, 2023.

Kundi la kwanza la wanajeshi wa Kenya, Uganda na Sudan Kusini liliabiri ndege Jumapili, Disemba 3, 2023 alfajiri jijini Goma kuelekea Nairobi.

Huku hayo yakijiri, mapigano bado yanaendelea kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23.

Share This Article