Wanajeshi Gabon wasema wanachukua uongozi

Marion Bosire
1 Min Read

Wanajeshi nchini Gabon wametangaza kwamba wanachukua uongozi wa taifa hilo.

Kwenye hotuba kupitia runinga, wanajeshi hao walisema wanatupilia mbali majibu ya uchaguzi wa Urais uliofanyika Jumamosi ambapo Rais Ali Bongo wa umri wa miaka 63, alitangazwa mshindi.

Iwapo watatekeleza tishio lao, watakomesha uongozi wa familia ya Bongo nchini Gabon wa miaka 53 sasa.

Wanajeshi 12 walionekana kwenye runinga leo Jumatano Agosti 30, 2023, ambapo walitoa tangazo hilo na kuongeza kwamba mipaka yote ya nchi hiyo imefungwa kwa muda usiojulikana.

Kwenye hotuba kupitia kituo cha runinga cha Gabon 24 wanajeshi hao walisema wameamua kulinda amani ya nchi yao kwa kukomesha uongozi wa sasa.

Walitaja uongozi huo kuwa usiowajibika na usiotabirika na umesababisha kuzorota kwa utangamano nchini humo hali ambayo inatishia kusababisha migogoro.

Awali, upande wa upinzani nchini Gabon ulikuwa umetangaza kwamba umeshinda kwenye uchaguzi wa urais hata ingawa matokeo rasmi ya uchaguzi hayakuwa yametangazwa.

Share This Article