Wanahabari kote nchini leo Jumatano wanafanya maandamano wakitaka serikali kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unalindwa na kuheshimiwa.
Maandamano hayo pia yanalenga kulalamikia ukatili wa polisi walioelekezewa baadhi ya wanahabari wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Jijini Mombasa, wanahabari kadhaa wamejitosa mitaani kushinikiniza kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na kubeba mabango yaliyoandikwa uanahabari si uhalifu.
Jijini Nairobi, wanahabari walikusanyika nje ya jengo la Nation Centre walikokusudia kuanzia kufanya maandamano yao kushinikiza kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Vikitangaza kufanywa kwa maandamano hayo leo Jumatano, Chama cha Wahariri nchini, KEG na kile cha wanahabari, KUJ vilitangaza kuwa itakuwa zamu ya wanahabari kuandamana kulalamikia ukatili wa maafisa wa polisi na kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Tangazo hilo lilifuatia kisa cha mwanahabari wa kampuni ya Mediamax kwa jina Catherene Wanjeri Kariuki kupigwa risasi na maafisa wa usalama mjini Nakuru wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Katibu mkuu wa KUJ Eric Oduor kupitia taarifa alilaani kisa hicho akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wa polisi aliowataja kuwa watepetevu kazini.
Aliitaka mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi IPOA kutekeleza uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya maafisa watakaopatikana na hatia.
Awali, Rais wa KEG Zubeida Kananu alihutubia wanahabari katika kituo cha polisi cha Karen walikofika kuhakikisha usalama wa mwanahabari mkongwe aliyetekwa nyara Macharia Gaitho.
Gaitho anasemekana kukamatwa na kudhulumiwa na maafisa wa usalama katika kile walichokitaja kuwa kisa cha kumdhania kuwa mtu mwingine ambaye anachunguzwa na polisi.
Polisi baadaye waliomba radhi wakisema walimkamata mwanahabari huyo kimakosa.
Ni wakati huo ambapo Kananu alitoa ilani ya siku saba akitangaza kuwa wanahabari leo Jumatano watafanya maandamano ya kulalamikia ukatili wa maafisa wa polisi.
Kumekuwa na visa kadhaa vya wanahabari kushambuliwa na kujeruhiwa wakati wakiangazia maandamano ya vijana wa Gen Z.