Huku wanahabari kote nchini wakijitokeza kwa maandamano kulalamikia ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya Gen Z, wanahabari wa Meru kwa uongozi wa chama chao almaarufu “Meru Press Club” walijitokeza kuandamana kwenye barabara za mji huo.
Msafara wa waandamanaji hao ulianzia kwenye stendi ya basi karibu na duka la jumla la Tuskys na kufika hadi kwenye afisi ya kamishna wa kaunti ya Meru ambako walipokelewa na naibu kamishna wa kaunti wa eneo la Imenti kaskazini Bi. Ondiria Ndeti.
Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho cha wanahabari wa Meru David Muchui, waliamua kujiunga na wenzao kote nchini katika kusimama na wanahabari walioumizwa na maafisa wa usalama wakati wa maandamano dhidi ya serikali.
Muchui alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Meru kuhakikisha upatikanaji wa habari muhimu za serikali kwa wanahabari ambao wanatatizika sana kupata habari hizo.
Wanahabari waliozungumza walionyesha kutoridhika kwao na jinsi maafisa wa usalama wanachukulia wanahabari kote nchini.
Wameitaka serikali kulipa vyombo vya habari madeni yote kwani kampuni nyingi za habari zimeshindwa kulipa wafanyakazi wao mishahara.
Ondiria Ndeti wakati akipokea malalamishi ya wanahabari hao aliwashukuru kwa kufanya maandamano ya amani huku akipongeza ushirikiano ambao umekuwepo kati yao na wawakilishi wa serikali kuu katika kaunti ya Meru.