Wanafunzi wawili wa vyuo vya elimu ya juu walioripotiwa kutoweka tarehe 27 mwezi Oktoba mwaka 2023, wameokolewa na maafisa wa polisi, baada ya kuwekwa mateka kwa siku kadhaa katika mtaa wa Kitengela kaunti ya Machakos.
Wanafunzi hao wawili, walihadaiwa na mshukiwa mmoja wa kike, walipatikana wakiwa wamefungiwa katika chumba kimoja cha kukodishwa.
Washukiwa wawili waliotambuliwa Brian Ombasa Omoso mwenye umri wa miaka 25 na Humphrey Hinga mwenye umri wa miaka 22, walitiwa nguvni katika operesheni ya kuwaokoa wanafunzi hao, iliyotekelezwa na maafisa wa polisi wa maswala ya jina DCI.
Kulingana na maafisa wa polisi, washukiwa hao walitaka kulipwa fidia ya shilingi milioni sita kutoka kwa wazazi wa wanafunzi hao.
Uchunguzi wa polisi ulibainisha kuwa, mshukiwa wa kike aliyejitambulisha kuwa Debbie Zablon, aliwahadaa wanafunzi hao wawili kukutana naye mjini Nairobi, kabla ya kuwakabidhi kwa washirika wake.
Bastola bandia, kisu, kadi za simu ya rununu na nambari za usajili wa gari inayoaminika kuwasafirisha wanafunzi hao, pia zilinaswa katika chumba hicho.
Msako dhidi ya mshukiwa huyo wa kike umeanzishwa.