Wanafunzi waliobobea KCPE 2023 washerehekea matokeo mema

Martin Mwanje
2 Min Read

Watahiniwa walionawiri katika mtihani wa KCPE wa mwaka 2023 waliendelea kusherehekea mafanikio yao katika mtihani huo katika sehemu mbalimbali nchini.

Mtahiniwa bora zaidi katika mtihani huo alikuwa na alama 428 kati ya alama 500.

Matoko ya mtihani huo yalitangazwa na hii leo Alhamisi na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Shangwe na vigelegele vilirindima katika shule ya Gilgil Hills Academy, kaunti ya Nakuru baada ya Emmaculate Wacheke kujizolea alama 427.

Wacheke alikuwa mtahiniwa bora katika kaunti ya Nakuru na yamkini wa pili kote nchini.

Mtahiniwa huyo anayelenga kuwa mtaalam wa nyurolojia amehusisha matokeo hayo mazuri na bidii ya mchwa masomoni.

Azima yake ni kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Alliance.

Kule Nandi, shule za msingi za umma zimewatala katika matokeo ya mtihani wa KCPE mwaka 2023.
Kwenye matokeo hayo, shule ya msingi ya Bishop Muge Memorial katika eneo bunge la Mosop ilitwaa ubingwa kwa kutoa wanafunzi wawili, Belinda Jepngetich na Calvin Jepchirchir waliozoa alama 422 huku wanafunzi 89 wakipata alama zaidi ya 400.
Katika eneo bunge la Tinderet, mwanafunzi Santos Kiprono wa shule ya msingi ya St. Mathew Maraba ameweka shule hiyo katika nafasi ya pili kwa kuzoa alama 420.
Sherehe na mbwembwe za aina yake pia zilitawala katika shule za msingi za Cheribisi na Roseve katika eneo bunge la Emgwen ambapo wanafunzi zaidi ya 17 katika shule ya Cheribisi walizoa alama 400 huku wa kwanza Victoria Jepkoech ambaye licha ya kumpoteza babake kwa ugonjwa wa saratani kabla tu ya mtihani wa KCPE, aliongoza kwa alama 412.
Shule ya Roseve nayo ikiwa na mwanafunzi wa kwanza Collins Kihima aliyeongoza kwa alama 416.
Katika kaunti ya Kiambu, sherehe zilitanda katika shule ya DePaul Austin Junior Academy baada ya wanafunzi kadhaa shuleni hapo kujizolea zaidi ya alama 400.
Mathalan, mwanafunzi Alaina Wangari alipata alama 418.
Katika kaunti ya Kericho, shule ya msingi ya Chemitan Academy pia iliandikisha matokeo mema huku Rehina Chepngetich akipata alama 424.
Taarifa kutoka kwa waandishi wetu Dennis Rasto, Ephantus Githua na Erick Kiplangat 
Share This Article