Wanafunzi wahimizwa kuchagua kozi kwa makini

Kbc Digital
2 Min Read

Wanafunzi wamehimizwa kuchagua kozi kwa umakini kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, KCSE.

Matokeo hayo huenda yakatangazwa wakati wowote kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Huku vijana zaidi ya milioni 4.5 nchini wakikabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu wamehimizwa kuchagua kozi zao kwa umakini ili kuwasaidia kushindana vyema kwenye soko la ajira.

Ili kujenga nguvukazi thabiti, Veronica Kamau, Mtaalamu wa Ukarimu, Utalii na Mahusiano ya Kimataifa, amewataka wanafunzi kuhakikisha kwamba kozi wanazochagua zitawawezesha kupata fursa za ajira kwenye soko la ajira linalozidi kuwa finyu.

Akizungumza wakati wa siku ya wazi ya Chuo Kikuu cha Zetech mjini Ruiru, kaunti ya Kiambu, mtaalamu huyo alielezea wasiwasi kwamba wanafunzi wengi huchagua kozi kwa shinikizo kutoka kwa marafiki na wazazi, lakini baadaye huishia kuacha masomo hayo pale mambo yanapokuwa magumu.

Aidha, ripoti zinaonyesha kuwa taasisi nyingi za elimu nchini kenya zinaendelea kutoa wahitimu wenye shahada ambazo haziendani na ujuzi unaohitajika katika uchumi wa sasa.

Kwa kuwa serikali imefanyia marekebisho mfumo wa elimu nchini kwa nia ya kuhakikisha mtaala na mafunzo yanayotolewa kwa wanafunzi yanakidhi mahitaji ya taifa kama ilivyoainishwa katika maono ya mwaka 2030, Dkt. Henry Kiogora, Mkuu wa Idara ya Biashara na Uchumi katika chuo hicho cha kibinafsi, alisisitiza umuhimu wa kubaini vipaji vya wanafunzi katika hatua za awali za elimu ili kuwawezesha kufuata taaluma zao na kuzitumia kikamilifu.

Taarifa yake Antony Musyoka 

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *