Rais William Ruto amesema wanafunzi milioni 4 watanufaika na mpango wa lishe shuleni. Idadi hiyo itaongezwa kutoka wanafunzi milioni 1.6 ambao wamekuwa wakinufaika.
Akizungumza Jumanne wakati wa kuzindua mpango wa lishe shuleni wa kaunti ya Nairobi katika shule ya msingi ya Roysambu, Rais alisema shilingi bilioni 5 zitatumika kutekeleza mpango huo.
“Lazima tumalize aibu ya njaa katika nchi yetu. Tutamakinika kuhakikisha mpango wa lishe shuleni umetekelezwa,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kwamba ni aibu kwa watoto kwenda shuleni na kufunga kwa sababu ya ukosefu wa chakula.
Wakati huo huo, Rais alisema serikali itajenga madarasa 3,500 katika kaunti ya Nairobi kwa gharama ya shilingi bilioni 3 huku akisikitika kwamba watoto wengi hawaendi shuleni katika kaunti ya Nairobi kwa sababu ya ukosefu wa maendeleo ya miundombinu shuleni.
Ki0ngozi wa nchi aliwasihi wabunge wa kaunti ya Nairobi wafanye mkutano kuamua jinsi ya kushughulikia maendeleo ya miundombinu shuleni.