Wanafunzi watatu wa shule ya wavulana ya malazi ya Ober katika kaunti ya Homa Bay wameripotiwa kufariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha matatu na lori katika eneo la Kibwon, kaunti ndogo ya Nyakach, kaunti ya Kisumu.
Wanafunzi wengine 19 walijeruhiwa wakati wa ajali hiyo iliyotokea wakati wanafunzi hao walikuwa wakielekea nyumbani kwa likizo ya mwezi Aprili baada ya kufunga shule.
Matatu hiyo ilikuwa ikisafirisha wanafunzi kuelekea kaunti ya Kisumu ilipogongana na lori hilo kilomita chache kutoka mji wa Sondu.
Utingo wa matatu hiyo naye pia alifariki.
Akiwaomboleza wanafunzi waliofariki, Gavana wa kaunti ya Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o amewataka polisi kuanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo chake.
“Ni bahati mbaya kwamba tumewapoteza vijana kama hao katika ajali ya barabarani ambayo ingeepukwa ikiwa madereva wa magari yote mawili wangechukua tahadhari inayotakikana na kuzingatia utaalam,” alisema Prof. Nyong’o kwenye taarifa.
“Ningependa kutoa wito kwa polisi kuanzisha uchunguzi wa kina mara moja juu ya ajali hii kubaini chanzo chake na kuchukua hatua stahiki kwa watu ambao makosa yao huenda yalisababisha ajali hii.”
Gavana huyo amewatakia nafuu wanafunzi waliolazwa hospitali wakiuguza majeraha yaliyotokana na ajali hiyo.
Ajali hiyo inatokea wakati wanafunzi wengi wiki hii wanaelekea nyumbani kwa likizo ya mwezi Aprili baada ya kukamilika kwa muhula wa kwanza wa masomo.
Miito imeanza kutolewa kwa madereva kuwa waangalifu ili kuepusha ajali za barabarani zinazoweza kuepukwa ikiwa watazingatia sheria za trafiki.