Waliokamatwa wakichafua jiji la Nairobi wapatiwa kazi kama adhabu

Marion Bosire
1 Min Read

Watu wapatao 30 ambao walikamatwa jijini Nairobi wakichafua mazingira kwa kutupa taka ovyo na hata kwenda haja ndogo walifikishwa mahakamani Jumanne ambapo walipatiwa adhabu ya kazi kwa jamii.

Kazi hizo wanazifanyia katika vituo vya umma kama vile katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City jijini Nairobi.

Maafisa wa serikali ya kaunti ya Nairobi wakiongozwa na afisa mkuu wa mazingira Geoffrey Mosiria, wamekuwa wakizuru barabara za jiji la Nairobi ambapo walikamata wakenya waliokuwa wakifanya makosa madogomadogo.

Sheria ya kero ya umma ya kaunti ya Nairobi ya mwaka 2021 imetoa adhabu ya faini ya shilingi elfu 10, kifungo cha miezi sita gerezani au vyote viwili kwa yeyote atakayepatikana akienda haja kubwa au ndogo katika sehemu za wazi.

Wakati wa pitapita ya maafisa hao wa serikali ya kaunti ya Nairobi, wanaochuuza vyakula na bidhaa nyingine walimulikwa kwa kutupa taka ovyo huku wakiagizwa kuiondoa.

Kulingana na Mosiria serikali ya kaunti ya Nairobi imeajiri watu kadhaa ambao wanasaidia kukamata wanaovunja sheria hiyo ya kero ya umma huku akiwataka wakazi wote kuwa makini.

Hatua hiyo alisema inadhamiriwa kuhakikisha jiji la Nairobi linakuwa safi.

Share This Article