Waliofuzu KIMC wahimizwa kuongoza mabadiliko ya kidijitali nchini

Waziri Ndung'u alikuwa mgeni wa heshima katika mahafali ya KIMC mwaka 2024

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali Dkt. Margaret Ndungu amehimiza waliofuzu kutoka Chuo cha Mawasiliano nchini, KIMC wawe mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini.

Akizungumza katika hafla ya mahafali ya chuo hicho, Dkt. Ndung’u aliangazia jukumu muhimu la wataalamu wa umri mdogo katika safari ya taifa hili ya mabadiliko ya kidijitali.

Aliwahimiza waliofuzu kukumbatia fursa nyingi zilizoko kwenye sekta inayobadilika kila siku ya uchumi wa dijitali.

Waziri huyo alikariri kujitolea kwa serikali kuwapa vijana uwezo kupitia kwa mipango kama “Jitume” unaowaunganisha na fursa za ajira mitandaoni na vituo vya kidijitali kote nchini.

Hata hivyo,  Dkt. Ndung’u alitahadharisha wahitimu hao kuhusu changamoto za usalama pamoja na habari za kupotosha mitandaoni huku akipendekeza uadilifu.

Alitangaza ujio wa mswada wa mwaka 2024 kuhusu chuo hicho cha mafunzo ya mawasiliano unaopendekeza jina lake libadilishwe na kuwa “Shule ya Mawasiliano nchini Kenya, yaani Kenya School of Communication”.

Hatua hiyo, kulingana naye, inadhamiriwa kuboresha mafunzo ya mawasiliano nchini, kukita utaalamu katika tasnia ya mawasiliano na kupiga jeki uchumi wa kiufahamu nchini.

Kadhalika lihimiza wahitimu hao pia kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha uvumbuzi na utofauti.

“Safari yenu inaanza leo. Tumieni sauti na talanta zenu kusaidia kuunda Kenya yenye jamii iliyoendelea kidijitali na jumuishi,” alimalizia Waziri Ndung’u.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *