Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwenye bajeti ya ziada kuwalipa fidia wakazi wa Gatundu Kaskazini walioathirka na ujenzi wa bwawa la Kariminu II.
Waziri wa Maji Zachary Njeru alisema wakazi 122 ambao ardhi yao na boma zinakabiliwa na tishio la kuzama kufuatia kujaa hadi pomoni kwa bwawa hilo watalipiwa fidia na kisha kuhamishiwa sehemu salama.
Akizungummza jana Jumatatu alipozuru bwawa hilo kutathmini hali baada ya shughuli ya uondoaji maji ya ziada kutoka bwawa hilo kuanza siku ya Jumamosi, Waziri alisema shughuli za kuwalipa fidia na kuwaondoa waathiriwa kutoka vijiji vya Iruri, Kiriko, Gathanji na Kanyoni imeanza.
Njeru wakati huohuo, alisema serikali itawapelekea maji kwenye maboma yao wakazi wanaoishi karibu na bwawa hilo lililojengwa kwa mabilioni ya pesa.
Wakazi walikuwa wameitaka serikali kuhakikisha wanasambaziwa maji kabla ya maji hayo kusambazwa katika sehemu nyingine kama vile Nairobi, Juja na Ruiru.
Aidha Waziri Njeru alipuzilia mbali dhana kwamba mabwawa mengine ya Sasumua na Ndakaini ni tishio kwa wakazi wanaoishi nyanda za chini akisema kwamba viwango vya maji kwenye mabwawa hayo vinaagaliwa.