Walimu wakubali matumizi ya AI kwa mafunzo ya kiingereza

Walimu wanahisi AI itaboresha mfumo wa kibinafsi wa kujifunza, kuwawezesha kushughulikia kazi za kila siku kwa urahisi na hivyo kuwapa muda zaidi wa kuhamasisha, kuungana na wanafunzi na kukuza mapenzi ya lugha hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read

Shule kote ulimwenguni zimeanza kuingiza teknolojia ya akili mnemba – AI katika mitaala yao ya kiingereza, hatua ambayo imezua msisimko, mijadala na mabadiliko makubwa.

Walimu wa kiingereza wamesifia teknolojia hiyo mpya kwa kuboresha mfumo wa kibinafsi wa kujifunza, kuwawezesha kushughulikia kazi za kila siku kwa urahisi na hivyo kuwapa muda zaidi wa kuhamasisha, kuungana na wanafunzi na kukuza mapenzi ya lugha hiyo.

Wakizungumza katika mkutano wa kimataifa wa kila mwaka uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Zetech, walimu wa kiingereza chini ya mwavuli wa Chama cha Wataalamu wa Lugha ya Kiingereza Kenya (ELPAK), walipuuza hofu kwamba ukuaji wa teknolojia hiyo utachukua nafasi ya walimu, wakisema badala yake, itawapa uwezo zaidi.

Walisisitiza kwamba AI sio dhana ya siku zijazo tena bali ni uhalisia wa sasa darasani, hasa katika mafundisho ya lugha ya Kiingereza.

Walimu wakiongozwa na Jemal Maringo kutoka Tanzania na Rukia Mohammed walieleza kwamba teknolojia hiyo mpya imekuwa msaidizi wa darasani kwani wengi wao hutumia AI kuchanganua maandishi ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi, hivyo kupata muda wa kufanya mafunzo ya mtu kwa mtu na mijadala ya maana.

Profesa Njenga Munene, makamu mkuu wa chuo kikuu cha Zetech, alielezea kwamba lugha ya Kiingereza ni muhimu kutokana na matumizi yake ya kimataifa, ikitumika kama lugha ya mawasiliano ya kimataifa, elimu na teknolojia.

Website |  + posts
Share This Article