Walimu wahimizwa kuwa waaminifu katika kusimamia mitihani ya kitaifa

Martin Mwanje
2 Min Read
Katibu katika Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang

Katibu katika Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang ametoa wito kwa walimu kurejesha imani ya jamii kwa kusimamia kwa uaminifu mitihani ya kitaifa mwaka huu. 

Amesema walimu kimsingi wanapaswa kuchukua karatasi za mitihani kutoka vituo vinavyotumiwa kuhifadhi mitihani hiyo, kuisimamia na kurejesha karatasi za majibu bila hofu kuwa watalemaza usimamizi wa mitihani hiyo.

“Tunapaswa kushughulikia mapungufu ya uaminifu ambayo yameibuka katika jamii kuhusiana na usimamizi wa mitihani ya kitaifa,” amesema Dkt. Kipsang.

Kulingana naye, walimu wanapaswa kusimamia mitihani hiyo namna madaktari wanavyowatibu wagonjwa bila kuwepo kwa maafisa wa usalama katika wodi au vyumba vya kuwafanyia wagonjwa upasuaji.

Dkt. Kipsang aliyasema hayo wakati wa mkutano na maafisa wa elimu na washikadau wengine katika shule ya upili ya Shimo la Tewa mjini Mombasa.

 Katibu huyo alisema wizara itaweka mikakati ya kuhakikisha hakuna visa vya udanganyifu katika mitihani inayofanywa humu nchini.

“Kama maafisa wanaosimamia mitihani ya kitaifa, tunapaswa kuwa macho na kuhakikisha hakuna visa vyovyote vya udanganyifu vinavyoshuhudiwa ili kuongeza uaminifu, uhalali na imani katika mitihani hiyo,” aliongeza Dkt. Kipsang.

Mitihani ya KCPE, KPSEA na KCSE inatarajiwa kuanza nchini mwezi Novemba na serikali imewahakikishia watahiniwa wote kuwa imejitayarisha vilivyo kufanikisha usimamizi wake.

Hii ni pamoja na kusafirisha kwa kutumia ndege karatasi na vifaa vingine vitakavyotumiwa katika usimamizi wa mitihani hiyo katika maeneo yatakayokumbwa na mvua za El Nino.

Mvua hizo zimetabiriwa kunyesha kati ya mwezi Oktoba na Disemba mwaka huu.

Share This Article