Walimu wa chekechea katika kaunti ya Machakos wanaitaka serikali ya kaunti hiyo itekeleze mpango wa huduma wakisema masharti ya sasa ya kikazi ni ya dhalimu na ya kukatisha tamaa.
Mwenyekiti wa chama cha Walimu wa chekechea nchini Lawrence Otunga,ambaye alizungumza kwenye mkutano na walimu wa chekechea wa kaunti ya Machakos alikashifu serikali ya kaunti kwa kutozingatia maelekezo ya tume ya mishahara SRC.
SRC ilielekeza kwamba kila mwalimu alipwe kulingana na kiwango chake cha masomo.
Otunga analaumu maafisa wa serikali ya kaunti kwa kuficha mpango wa huduma wa walimu akionya kwamba iwapo serikali ya kaunti haitachukua hatua, walimu wataandamana hadi kwenye afisi ya Gavana kushinikiza hilo.
Kulingana naye, walimu wa chekechea wa Machakos wamedunishwa na kudhalilishwa huku wengi wakishindwa kulipa mikopo waliyochukua kutoka benki hata baada ya kuahidiwa kupatiwa barua za ajira lakini hawajazipokea hadi sasa.
Kuhusu mpango wa lishe shuleni ulioanzishwa na serikali ya kaunti Januari, 2024 katika vituo vyote vya elimu ya chekechea, walimu walilalamikia kulazimishwa kusafirisha chakula kutoka kwenye maghala.
Walimu hao ambao wamepatiwa jukumu la kubeba mchele, maharagwe na maziwa kutoka vituo hivyo hadi shuleni wanasema ni aibu na jukumu hilo linaingilia utendakazi wao.
Mwenyekiti wa chama cha walimu wa chekechea kaunti ya Machakos Hellen Musyoki alielezea kutoridhika kwake idadi ya walimu walioko ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi.
Hali ilivyo sasa kulingana na Musyoki mwalimu mmoja anahudumia wanafunzi zaidi ya 80 katika darasa moja huku akihimiza Gavana wa kaunti hiyo asikie kilio chao.
Grace Nzioki, aliyeajiriwa kwa mkataba wa mwaka mmoja anahofia kwamba mkataba huo utafikia mwisho hivi karibuni na anaomba Gavana kuongeza muda wa mikataba yao au awape ajira ya kudumu.
Walimu hao wanashangaa ni kwa nini hawaajiriwi kwa masharti ya kudumu kama wenzao wa kaunti za Makueni na Taita Taveta ilhali kuna raslimali za kutosha.