Walimu kuogelea kwenye hela kuanzia mwezi huu

Martin Mwanje
2 Min Read
Maafisa wa TSC, KNUT na KUPPET wakiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wao Jumatatu

Walimu katika shule za umma watapopokea nyongeza ya mshahara ya kuanzia asilimia 7 hadi 10 kama ilivyotangazwa na Rais. 

Walimu wataanza kupokea nyongeza hiyo katika mishahara yao ya mwezi huu wa Agosti ambayo itajumuisha malimbikizi ya kuanzia Julai 1, 2023.

Hii inafuatia mazungumzo yaliyofanyika kati ya Tume ya Walimu, TSC na vyama vya walimu vya KNUT na KUPPET leo Jumatatu.

TSC pamoja na vyama hivyo vimesaini makubaliano mengine kwa lengo la kuufanyia mabadiliko Mkataba wa Pamoja wa Maelewano, CBA wa mwaka 2021-2025.

Makubaliano hayo yanalenga kuwakinga walimu dhidi ya matozo mapya ya serikali na gharama ya juu ya maisha.

Chini ya makubaliano hayo, mshahara wa msingi wa walimu utaongezwa hadi asilimia 9.5 itakayolipwa katika kipindi cha miaka miwili ya fedha kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Mshahara wa msingi wa walimu walio katika kundi la C2 ambalo linajumuisha walimu walioajiriwa punde baada kuhitimu vyuoni watapokea nyongeza ya hadi shilingi 4, 164, wale walio katika kundi la C3 watapokea nyongeza ya shilingi 5,141 ilhali wale walio katika kundi la D5 watapokea nyongeza ya shilingi 4,883.

Wakati wa mazungumzo hayo, KUPPET ilipinga vikali hatua ya Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC ya kuwekea ukomo mshahara wa walimu walio katika kundi la C5. Pande zote mbili zitaangazia upya suala hilo punde baada ya kushirikishana data kulihusu.

Marupurupu ya nyumba kwa walimu wanaofanya kazi katika sehemu za mashambani na miji midogo pia yamepitiwa upya.

Katika mapitio hayo, marupurupu ya nyumba ya walimu walio katika kundi la C3 na C4 yamelinganishwa huku zoezi kamili la ulinganishaji likitarajiwa kumalizika mwezi Julai mwaka ujao.

Asilimia 87 ya walimu wanapokea marupurupu ya nyumba katika kundi la C4, hawa wakiwa walimu ambao hasa wanahumu katika maeneo ya mashambani.

Kwa mujibu wa maipitio hayo, marupurupu ya walimu wanaohudumu katika sehemu za mashambani na miji midogo yataongezeka kwa shilingi 2,100 kila mwezi kwa walimu walio katika kundi la C2 ilhali walimu walio katika kundi la D4 watapokea nyongeza ya mshahara wa shilingi 8,700 kwa mwezi.

 

Website |  + posts
Share This Article