Wakulima humu nchini wametakiwa kuwa waangalifu wanaponunua mbegu ya mahindi wakati huu wa upanzi.
Wataalamu wa kilimo wameonya kuwa biashara haramu ya mbegu ghushi inatishia pakubwa uzalishaji wa zao la mahindi katika kaunti ya Trans Nzoia msimu huu wa upanzi, hali inayohatarisha usalama wa chakula nchini ikizingatiwa kuwa kaunti hiyo inazalisha zaidi ya magunia million tano ya mahindi kila mwaka.
Akizungumza mjini kitale katika kikao na wadau mbalimbali wakati wa halfa ya mashindano ya gofu, mkurugenzi wa kampuni ya mbegu nchini (Kenya Seed) Sammy Chepsiror, amesema kwamba biashara ya mbegu ghushi inaendelea kuwa donda sugu kwa uzalishaji wa chakula na kutaka serikali na vitengo husika kukaza kamba kuhakikisha biashara hiyo inayoshika kasi kila msimu wa upanzi inakoma.
Mkurugenzi huyo amewataka wakulima kujikakamua na kuhakikisha wanapata mbegu bora na kushiriki kilimo msimu huu ambapo asilimia 75 ya vyakula hupandwa.
Chepsiror amekariri kuwa kampuni hiyo bado inasubiri shilingi bilioni moja kutoka kwa serikali kuu kufanikisha mpango wa ruzuku ya mbegu na kuhakikisha kampuni hiyo haipati hasara kutokana na gharama ya uzalishaji.