Waziri wa Kilimo Mithika Linturi anasema wakulima kote nchini wanatarajia kupata mavuno mengi kufuatia usambazaji uliofanikiwa wa mbolea ya bei nafuu uliofanywa na serikali.
Linturi ameiagiza Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao, NCPB kufungua vituo vipya vya kuuzia mbolea hiyo karibu na raia na kuwaajiri vibarua kusimamia vituo hivyo.
Hii ni kutokana na mashaka kwamba baadhi ya wakulima walishindwa kupata mbolea ya bei nafuu kutokana na gharama za juu za usafiri.
Linturi amesema vibarua hao watakuwa kiungo muhimu katika usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kabla ya kuanza kwa msimu mfupi wa mvua.
Waziri aliyasema hayo alipofika mbele ya Kamati ya uwekezaji ya Bunge la Taifa inayoongozwa na mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe.
Serikali imetangaza kuwa bei ya mbolea ya bei nafuu itapunguzwa kutoka shilingi 3,500 hadi 2,500 katika hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa mavuno mengi na hivyo kuihakikishia nchi usalama wa chakula katika siku zijazo.