Vyama kadhaa vya ushirika vya wakulima katika kaunti ndogo ya Matungulu, kaunti ya Machakos vimeungana na kutoa wito kwa idara ya upelelezi wa jinai DCI na polisi kuchunguza jamaa aliyejitangaza kuwa mratibu wao.
Wakulima hao wanasema kwamba Cyrus Mutunga Masaku, alijiteua kuwa mratibu wao na anadai kuwa na uhusiano wa karibu na Rais William Ruto na waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen.
Amekuwa akitumia madai hayo kuwahadaa wakulima hao akiwaahidi kwamba atatumia ushawishi wake kutatua shida zinazokabili vyama vyao na kuwawezesha kupokea hatimiliki za ardhi haraka.
Vyama hivyo vinajumuisha Kwa Matingi, Kimiti, Muka mukuu, Kayatta, Matuu Wendano, Kyaume, Mwatati na vingine.
James Mwovi Mwangangi ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Kwa Matingi alielezea kwamba Mutunga amekuwa akizunguka na kuwapora viongozi waliochaguliwa wa vyama hivyo pesa.
Mwovi aliendelea kusema kwamba Mutunga anadai kwamba alichaguliwa na wakulima wa Matungulu kuwa mratibu wao na ameishia kuwapunja.
Wakulima hao sasa wanataka kufahamu ukweli kumhusu Cyrus Mutunga Masaku, anakofanya kazi na iwapo kweli ana ushawishi anaodai.
Gerald Kiswii mwenyekiti wa chama cha Kimiti alielezea kwamba jamaa huyo alichukua zaidi ya shilingi laki moja kutoka kwake wakati mmoja na baadaye akaitisha shilingi elfu 130 ili kusaidia kupata hatimiliki ya ardhi ya chama hicho.
Baada ya hapo alikata mawasiliano na hakuwahi kurejea katika afisi za chama hicho.
Phillip Muli Munyaka mwanachama wa chama cha Matuu Wendano anasema Cyrus Mutunga alijitambulisha kwake kama mfanyakazi wa afisi ya Rais na baada ya mashauriano wakaafikiana ampe laki 4.
Cyrus Mutunga Masaku tayari amekanusha madai kwamba yeye ni mratibu wa vyama vya ushirika vya wakulima Matungulu akisema anatoa huduma hizo katika chama cha Matuu Wendano pekee.
Kuhusu ushawishi katika Ikulu, Afisi ya Rais na uhusiano na Waziri Murkomen, Mutunga alikosa kuelezea wazi akisema marafiki wake ni suala la faragha ambalo halifai kuhusishwa na masuala ya vyama hivyo.
Alikanusha madai ya kulaghai wanachama pesa akitaka suala hilo liwasilishwe kwa maafisa wa polisi kwani yeye tayari ameandikisha taarifa kwa polisi kama walivyofanya viongozi wa vyama hivyo.