Rais William Ruto amesema kwamba wakulima katika maeneo yanayozalisha kiwango kikubwa cha chakula nchini kama Trans Nzoia watapokea mbolea ya bei nafuu kuanzia wiki ijayo.
Huku akitaja hatua hiyo kama sehemu ya mpango wao wa kupiga jeki uzalishaji, Rais alisema kufuatia upatikanaji wa pembejeo kwa bei rahisi, wanalenga mavuno ya magunia milioni 80 ya mahindi mwaka huu.
Kiongozi wa nchi alikuwa akizungumza wakati wa kuzindua mradi wa maji wa Kiptogot-Kolongolo katika kaunti ya Trans Nzoia.
Mradi huo utatoa maji kwa zaidi ya watu elfu 150 wanaoishi katika maeneo ya Kaptega, Kiptogot, Twiga, Chorlim, Endebess, Kwanza, Kapkoi, Kapomboi, Kobos na Kolongolo.
Rais alihutubia mikutano ya hadhara katika vituo vya kibiashara vya Chepchoina na Mowlem akiwa ameandamana na Gavana George Natembeya, mawaziri Zacharia Njeru wa maji na Susan Nakhumicha wa afya, wabunge kadhaa na wawakilishi wadi.
Gavana Natembeya alimkaribisha Rais Ruto katika kaunti ya Trans Nzoia akisema kaunti hiyo inatafuta kushirikiana na serikali ya kitaifa katika utekelezaji wa miradi muhimu.