Rais William Ruto amesema serikali imejitolea kuifanyia sekta ya maziwa mabadiliko ili kuongeza mapato ya wakulima.
Amesema serikali inatumia shilingi bilioni 5 kuweka mitambo ya kisasa katika kampuni ya New Kenya Co-operative Creameries (KCC) ili kuboresha utendakazi wake kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wakulima.
Alieleza kuwa dhamira ni kuongeza uwezo wa uchakataji maziwa wa kampuni ya KCC ili kuhakikisha inachakata maziwa yote yanayozalishwa na wakulima.
Rais aliiagiza kampuni ya KCC kuanza kuwalipa wakulima wa maziwa shilingi 50 kwa lita kuanzia Machi mosi mwaka huu na kuhakikisha bei hiyo haitayumba kamwe.
“Kuanzia Julai 1, wakulima watalipwa kila baada ya siku 15. Hivyo ndivyo tutakavyoangamiza uchuuzi wa maziwa unaotokea wakati wakulima wanakosa kulipwa kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu,” alisema kiongozi wa nchi.
Aliyasema hayo jana Jumatano wakati wa uzinduzi wa kampuni ya New KCC mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia.