Gavana wa kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga amezindua mpango wa usambazaji wa mbegu za mtama kwa lengo la kukabiliana na athari za ukame.
Kilo hizo 9,350 za mbegu za mtama zenye thamani ya shilingi milioni 6.5 zitagawiwa wakulima katika kaunti ndogo za Ndhiwa, Suba Kusini na Suba kaskazini.
Mbegu hizo zinajumuisha kilo 7,850 za aina ya Gadam ambazo mazao yake yatauziwa kampuni ya kuandaa mvinyo ya East African Breweries Limited na nyingine 1,500 aina ya Seredo ambazo mazao yake yatatumiwa kwa chakula.
Kando na mbegu, usaidizi huo unajumuisha lita 1200 za dawa za kuua minyoo na chanjo za thamani ya shilingi milioni 1.2 pamoja na pesa taslimu milioni 18 ambazo zitafaidi familia 1500.
Mpango huo unaofadhiliwa na shirika la Ujerumani kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Homa Bay, Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na Kilimo, FAO, serikali ya kitaifa na wakfu wa First Bridge ambao unatekeleza mpango huo mashinani, utafaidi wadi 11.
Wadi hizo ni Ruma Kaksingri Mashariki, Kaksingri Magharibi, Gwassi Kaskazini, Gwassi Kusini, Lambwe, Gembe, Kosewe, South Kabuoch, Kanyikela, Kanyadoto na Kwabwai.
Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha jamii thabiti ambayo inajitegemea katika eneo hilo.