Baraza la taifa kuhusu kilimo cha viazi (NPCK), linalenga kuwahusisha wakulima 150,000 wa viazi katika katika kaunti nne zinazokuza viazi nchini, ili kuongeza kasi ya ukuzaji zao hilo, kupitia mradi wa ustawishaji viazi nchini KSPI.
Kaunti hizo ambapo mradi huo utatekelezwa ni pamoja na Nyandarua, Nandi, Laikipia na Meru.
Ili kuhakikisha mradi huo unafaulu, baraza hilo la taifa la viazi, pia litashirikiana na taasisi ya utafiti wa kilimo na mifugo (KALRO) tawi la Tigon, Chuo kikuu cha Egerton, kituo cha AGRA, Simplifine na Viazi Kings.
Wakati wa uzinduzi huo mjini Ol Kalau kaunti ya Nyandarua, afisa mkuu mtendaji wa NPCK Wachira Kaguongo, alisema mradi huo utaharakisha zao la viazi katika kaunti hizo kuanzia upanzi hadi mauzo.
“Mbali na kuwahusisha wakulima hao 150,000, mradi huo pia unalenga kuwafikia wakulima wengine 300,000, pamoja na kutoa nafasi 5,000 za kazi kwa vijana na wanawake,” alisema Kaguongo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo cha AGRA hapa nchini John Macharia, alisema uzalishaji wa viazi hapa nchini unafuata ule wa mahindi, na hali hiyo itaimarishwa hata zaidi.
Waziri wa kilimo kaunti Nyandarua Samuel Gitaka, alisema erikali ya Nyandarua imeanzisha kituo cha kuzaliza mbegu za viazi, ili kuimarisha kilimo cha zao hilo.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wadau wengine wa kilimo cha viazi kutoka kaunti zingine.