Wakongwe ambao hupokea pesa za matumizi kutoka kwa serikali kila mwezi chini ya mpango wa “Inua Jamii” wameitaka serikali kutafakari kuhusu kuongeza mgao wa kila mwezi ili waweze kujikimu nyakati hizi ngumu kiuchumi.
Wazee hao wa umri wa miaka 70 na zaidi, mayatima na walemavu hupokea shilingi elfu 2 kila mwezi chini ya mpango huo wa serikali kuu.
Pesa hizo huwasaidia kununua chakula na dawa lakini wazee waliohojiwa huko Ruiru wanataka pesa hizo ziongezwe hadi shilingi elfu 4 kwa kila mmoja kwani elfu mbili za sasa hazitoshi kugharamia mahitaji yao ya kila mwezi kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za msingi
kama chakula.
Wakizungumza katika ukumbi wa jamii huko Ruiru Social wakati wa shughuli ya kufungulia wazee waliosajiliwa kwa mpango huo akaunti za benki, wazee hao walisema wamekuwa wakitegemea watoto wao kwa mahitaji mbali mbali na sasa baadhi ya watoto hao wamepoteza ajira na hata kufunga biashara.
Tegemeo lao sasa ni mpango huo wa Inua Jamii.
Mbunge wa eneo la Ruiru Simon Ng’ang’a King’ara ambaye alizindua mpango wa kuwafungulia wazee akaunti za benki alisihi wazee watumie fursa iliyotolewa na serikali kuhakikisha akaunti zao ziko sawa ili waendelee kupokea pesa zao.
King’ara alisema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba pesa hizo hazicheleweshwi, na inafanya juhudi pia za kulinda mpango wa Inua Jamii dhidi ya walaghai ambao wamekuwa wakisajili watu wasiojulikana ili kupora pesa hizo.
Serikali kupitia kwa wizara ya Leba na Utunzaji jamii inasajili watu zaidi kwenye mpango wa Inua Jamii, mwendelezo wa mpango ulioanza Septemba 2023 ambapo watu zaidi ya elfu 500 walisajiliwa.
Rais William Ruto aliahidi kuongeza wanaofaidika na mpango huo hadi milioni 2.5 kwa awamu.