Wakili wa Rigathi Gachagua Elisha Ongoya amechukua hatua kuhusu ujio wa akaunti nyingi za mitandao ya kijamii zilizofunguliwa na watu wanaojisingizia kuwa yeye.
Akaunti hizo zipatazo 58 zina jina lake au picha yake kwenye utambulisho na ameziripoti kwa mamlaka ya mawasiliano nchini CAK na idara ya upelelezi wa jinai DCI zichunguzwe.
Ongoya anaiomba CAK ifunge akaunti hizo kwa ushirikiano na kampuni zinazomiliki na kuendesha mitandao ya kijamii kwa lengo la kuzuia uenezaji wa habari zisizo za ukweli.
Wakenya wengi walipata kumfahamu Ongoya kupitia kwa kikao cha bunge la seneti cha kusikiliza kesi ya kumbandua madarakani Rigathi Gachagua.
Mawakili wa Ongoya wanasema kwamba akaunti 48 zimefunguliwa kwa jina lake kwenye mtandao wa X, saba kwenye Facebook na tatu kwenye TikTok.
Wanadai kwamba yanayochapishwa kwenye akaunti hizo hayaambatani na falsafa ya maisha yake na mengine yanafanana uhalifu.
Mawakili hao wa Ongoya vile vile wanahisi kwamba akaunti hizo huenda zikamchafulia jina na hivyo wanataka hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti hali.