Kaunti ya Lamu ni mojawapo ya kaunti za Pwani ambazo uraibu wa madawa ya kulevya umeendelea kuwa tishio miongoni mwa kizazi cha sasa na licha ya asasi husika kuweka mikakati ya kudhibiti jinamizi hili, bado azimio la kutatua tatizo hili halijaafikiwa vikamilifu.
Kulingana na ripoti ya mwaka wa 2022 ya Shirika la kupambana na utumizi wa dawa za kulevya na vileo haramu nchini NACADA, mkoa wa pwani uliongoza kwa matumizi ya zaidi ya dawa mbili za kulevya kwa wakati mmoja.
Lakini je, wenyeji na makundi yasiyo ya kiserikali yanafanya juhudi gani katika kusaidia serikali kuzuia ueneaji zaidi ?
Wakfu usio wa faida wa Waridi Foundation chini ya mkurugenzi mtendaji Jenniffer Wairimu umekuwa kipaumbele katika juhudi za kuwaleta vijana pamoja na kutoa hamasa juu ya madhara ya dawa za kulevya.
Vile vile kuwashirikisha katika michezo tofauti tofauti kama njia moja ya kuwaepusha kujihusisha na uraibu wa madawa ya kulevya.
Siku ya Jumapili Agosti 6, Wakfu huu uliandaa mashindano ya raga ya Lamu 7 Sevens yalioleta pamoja timu kadha wa kadha kutoka eneo la Lamu. Mchezo wa Raga katika eneo hili umeanza kuwa mchezo pendwa miongoni mwa wana rika siku za hivi karibuni.
Timu zilizoshiriki mashindano hayo ni Mpeketoni Boys, Black warriors, Tiger A, Tiger B, Witu mjini, Witu NYS, na Witu Sharks.
“Nilianza kuandaa mashindano haya ya Lamu 7s mwaka wa 2016 wakati nikiwa Miss Tourism Lamu” alisema Wairimu, ilikuwa ni fursa ya kipekee hapa Lamu na njia ya kipekee ya kuwapa vijana kitu cha kufanya ili kuwaepusha kujihusisha na ulanguzi wa madawa ya kulevya,” Jenniffer Wairimu aliendelea.
Kwenye michuano iliyoshamiri ufundi na maarifa ya mchezo timu ya sekondari ya Mpeketoni iliibuka mshindi kwa alama 12 dhidi ya7 za Tiger A katika fainali ya mashindano ya Raga ya LAMU 7s na kushinda taji lenye dhamani ya shilingi. 50,000.
mashindano hayo yalihudhuriwa na wachezaji tajika wa Raga kama vile Martin Owillah wa KCB na Leon Lubhaga wa Kenya Rugby Union.
“Shukrani za dhati kwa OCS wa kituo cha polisi cha Mpeketoni NGUNJIRI kwa kutushika mkono na kuhakikisha kwamba vijana wana uhusiano mwema na askari na kwamba wanaweza wakatoa taarifa ya utovu wa usalama ambao umekithiri bila kuogopa,” Mkurugenzi mtendaji alimshukuru mkuu wa polisi eneo hili huku akitoa shukrani kwa wote waliohudhuria.
NI KWELI MICHEZO INASAIDIA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA?
Wataalamu wa michezo wanakubali kwamba inawezekana kutumia michezo kama chombo cha kuzuia uhalifu na utumiaji wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana mahali popote kwa kuzingatia mbinu, sera na miundo mbinu mwafaka.
Mtaalamu wa maswala ya michezo na sayansi na aliyekuwa naibu gavana wa kaunti ya Lamu kwa wakati mmoja Eric Mugo katika kikao na wanahabari Septemba, mwaka wa 2021 alisema michezo hutoa mafunzo ya stadi za maisha ambayo humpa mtu ujasiri dhidi ya tabia hatarishi na zisizo za kijamii.
“Vijana lazima waone maisha kutokana na michezo. Kadiri michezo inavyofanywa zaidi kwa tafrija na burudani, tunahitaji kuiangalia kama uwekezaji na kuwa na ramani ya muda mrefu. Haipaswi kuwa ya msimu.” alisema Mugo.