Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amesema kila Mkenya hivi karibuni ataifahamu sera ya kigeni ya nchi hii.
Ameitaja sera hiyo ambayo kwa sasa inapigiwa msasa kuwa ya “kigeni” kwa Wakenya.
Punde mchakato wa kukusanya maoni ya wadau na kuipigia sasa utakapokamilika, sera hiyo inatamzamiwa kukabidhiwa Rais William Ruto kwa ajili ya uzinduzi wake baadaye mwaka huu.
“Seya ya kigeni ya Kenya ambayo imekuwa ni ya “kigeni” kwa Wakenya sasa itamilikiwa na wananchi,” alisema Mudavadi wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya umma juu ya sera hiyo uliofanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC leo Jumatatu.
“Hii ni kwa sababu dhamira kuu ya sera ya kigeni ya nchi imejikita ndani ya matamanio ya wananchi wake yaliyomo katika “Sera ya Jamii yote ambayo inaakisi maoni, maslahi na maadili ya wananchi.”
Kwa misingi hiyo, Waziri huyo ameitaja sera ya kigeni kuwa waraka muhimu unaopaswa kuakisi, kuonyesha, kukuza na kulinda maslahi ya taifa la Kenya katika ushirikiano wa kimataifa.