Wakenya watumbuizwa kwa njia ya kipekee na DJ Afro

Marion Bosire
1 Min Read

Dj Afro anafahamika sana kwa namna ya kusisimua ambayo amekuwa akitafsiri filamu za mapigano na kuuzia wakenya.

Mbunifu huyo alihusishwa kwa mara ya kwanza kwenye burudani ya sikukuu leo kwenye maadhimisho ya sikukuu ya Jamhuri.

Burudani yake fupi ilihusu vipindi vya runinga ambayo vimekuwa vikisisimua wakenya kwa miaka kadhaa Kenya inapoadhimisha miaka 60 ya Uhuru.

Alianzia vipindi vilivyokuwa vikionyeshwa awali katika runinga ya KBC kama vile Tahamaki, vituko, Je huu ni ungwana na Tausi.

Mmoja wa wahusika wa kipindi Tausi ambaye alikuwa akiigiza kama Rehema alikuwepo uwanjani ambapo alizungumza maneno machache akitaja wahusika wengine kama Lindi.

Afro alikumbuka Marehemu Mzee Ojwang ambaye alikuwa mhusika mkuu katika kipindi cha Vitimbi na vioja mahakamani waigizaje wake wakiwakilishwa na Ondiek na Makokha.

Papa Shirandula ambaye aliaga dunia naye alikumbukwa huku wahusika wa kipindi hicho wakiwakilishwa na Wilbroda.

Katika maneno yake mwigizaji huyo ambaye jina lake halisi ni Jackie Nyaminde alimtania kiongozi wa nchi akisema kwamba yeye ni mpweke amkumbuke.

Vipindi vingine vilivyotajwa ni Mother Inlaw na Churchill Show.

Waigizaji wa mitandaoni ambao ndio wa nyakati za sasa nao hawakuachwa nyuma wakiwakilishwa na Manzi wa Facebook na Papa Fred.

Share This Article