Wakenya watakiwa kujitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura

Usajili ulioimarishwa wa wapiga kura, uliozinduliwa leo Jumatatu katika kaunti ya Kwale, unalenga kusajili wapiga kura wapya milioni 2.5 kufikia Aprili 28, 2026.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon akiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa usajili wa wapiga kura

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewataka Wakenya wanaotimiza vigezo vya kujisajili kama wapiga kura kufanya hivyo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon amesema wanalenga kusajili wapiga kura wapya milioni 2.5 katika zoezi lililozinduliwa leo Jumatatu la usajili ulioimarishwa wa wapiga kura nchini.

Zoezi hilo, lililozinduliwa katika kijiji cha Shimoni, eneo bunge la Lunga Lunga, kaunti ya Kwale, litamalizika Aprili 28.

Hata hivyo, zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura litaendelea katika afisi za tume hiyo kote nchini baada ya hapo.

Ethekon, aliyezungumza wakati akiwa ameandamana na makamishna wa IEBC na Gavana wa Kwale Fatuma Achani, amesema tume hiyo inalenga kuwasajili jumla ya wapiga kura milioni 28.5 kufikia mwaka 2027.

Ili kutimiza hilo, ametoa wito kwa washikadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa kisiasa na kidini, kuwa mstari wa mbele kuwarai wanaostahiki kujiandikisha kama wapiga kura kufanya hivyo ili sauti zao zisikike katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa IEBC alisema usajili wa wapiga kura hautafanywa katika maeneo ambako uchaguzi mdogo unatarajiwa kuandaliwa.

Maeneo hayo ni pamoja na eneo bunge la Samburu Magharibi na Emurua Dikkir.

Aidha, uandikishaji wapiga kura hautafanyika katika eneo bunge la Ol Kalou kufuatia kifo cha mbunge wa eneo hilo David Njuguna.

 

Share This Article